Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa zilizoenea katika mitandao ya kijamii hususan Facebook na WhatsApp zilizoainishwa kama “Tuhuma Nzito katika Tasnia ya Sheria”. Kwa ufupi, tuhuma hizo zinadai kuwa baadhi ya Wahadhiri na Watumishi wa Taasisi hii wanafanya “biashara haramu” ya kufelisha wanafunzi kwa makusudi sambamba na ubadilishaji wa matokeo ya mitihani, hususan Somo la Mirathi (Probate, Administration of Estates and Trusts).
Ufafanuzi:
Tunapenda kuufahamisha Umma kuwa tuhuma hizo si za kweli. Kumbukumbu zetu zinaonyesha kuwa wanafunzi wote waliofanya mitihani wametendewa haki. Wale waliofaulu wamefaulu kihalali na hakuna aliyefelishwa kwa makusudi. Katika utendaji kazi wa Taasisi watumishi wote wanafanya kazi kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
Kwa nafasi hii, tunapenda kueleza juu ya utaratibu wa utayarishaji na utoaji wa matokeo ya mitihani kama ifuatavyo:-
- Baada ya mtihani kusahihishwa na jopo la Wahadhiri wa somo husika (Internal Examiners), majibu ya wanafunzi (answer books) hupelekwa kwa Mtahini wa Nje ya Taasisi (External Examiner) kwa ajili ya uhakiki wa usahihishaji na alama za ufaulu zilizowekwa.
- Baada ya kupokewa kutoka kwa Watahini wa Nje na kuandaliwa, matokeo huwasilishwa katika kikao cha ndani cha Wahadhiri/Watahini wa Ndani (Panel of Internal Examiners) kwa ajili kujadiliwa na kutolewa mapendekezo ya kuwasilishwa katika Kamati ya Mafunzo kwa Vitendo na Mitihani (Practical Legal Training and Examinations Committee).
- Baada ya kupokelewa, kujadiliwa na kupitishwa na Kamati ya Mafunzo kwa Vitendo na Mitihani, Taasisi hutangaza Matokeo ya Awali (Provisional Results) kupitia Tovuti ya Taasisi ambayo inaruhusu mwanafunzi husika kuona matokeo yake baada ya kuingiza nambari yake ya usajili.
- Katika hatua ya mwisho, Matokeo ya Awali huwasilishwa kwenye Bodi ya Uendeshaji wa Taasisi (Governing Board) kwa ajili ya kujadiliwa na kuthibitishwa kuwa matokeo rasmi (Final Results).
Baada ya matokeo ya awali kutangazwa, mwanafunzi ambaye hajaridhika na matokeo yake ana haki na fursa ya kuomba uhakiki wa matokeo yake (verification) au kukata rufaa (appeal) au vyote kwa pamoja. Uhakiki humwezesha mwanafunzi husika kuthibitisha usahihi wa matokeo yake.
Hivyo, Taasisi inatoa rai kwa mwanafunzi ye yote ambaye ana shaka na matokeo yake kuwa afuate taratibu zilizoelezwa hapo juu.
Mwisho, Taasisi inatoa rai kwa wahusika waliotoa taarifa hizo za uzushi kuepuka tabia ya kutoa tuhuma bila ushahidi. Tuhuma zilizotolewa zimeleta usumbufu mkubwa sio tu kwa wahadhiri, wafanyakazi na wanafunzi wa Taasisi bali pia kwa wazazi/walezi wa wanafunzi na wadau wengine katika tasnia ya Sheria.
IMETOLEWA NA:
MKUU WA TAASISI TAASISI YA MAFUNZO YA UANASHERIA KWA VITENDO TANZANIA
(THE LAW SCHOOL OF TANZANIA)
5 Mei, 2015
Post a Comment